Burundi imewaandalia Watanzania vibali vya biashara, yasema TanTrade

Burundi imewaandalia Watanzania vibali vya biashara, yasema TanTrade

Na David  Nawepa

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) leo  (Septemba 7,2017)imewaalika wafanyabiashara wa Tanzania kupeleka bidhaa Burundi kwani tayari Wizara ya Biashara ya Burundi imekwishaandaa vibali vya biashara kwa ajili yao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari,  Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Bwana Edwin Rutageruka, amewahakikishia pia  wajasiriamali kwamba hali ya usalama Burundi ni nzuri na inaruhusu kufanya biashara nchini humo.

“Tayari tumezungumza na Wizara ya Biashara nchini Burundi  (juu yavibali na kuhakikishiwa kuwa) vibali vya kufanya biashara vimeshaandaliwa, hivyo bebeni bidhaa zenu. Katika mpango huu tumeshirikiana na TFDA, TBS, Uhamiaji, VAT na TIC kwa hiyo kila kitu kitafanyiwa kazi kulingana na mahitaji,” amehakikisha Bw. Rutegaruka.

Kaimu Mkurugenzi  Mkuu huyo amesema   ili kujiridhisha juu ya suala la usalama, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imefanya utafiti na kubaini kuwa hali nchini Burundi ni salama.

Bw Rutageruka ameeleza kuwa Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Bw Rajab Gamaha, amehakikisha kwamba Burundi ni salam, na kuongeza: “Balozi Rajab Gamaha anayetuwakilisha Burundi alikuja tukafanya naye mazungumzo: TanTrade na TPA, akatueleza namna fursa za kibiashara na uwekezaji zilivyo nyingi.”

Bw. Rutegaruka amesema  maandalizi ya mwisho ya kongamano la kibiashara kati ya Tanzania na Burundi litakalofanyika jijini Bujumbura yako ngazi ya mwisho. Kongamano hilo litafuatiwa na maonyesho ya biashara yatakayofanyika katika viwanja vya Tempete.

“Usafiri wa mabasi upo.  Basi la kampuni ya Adventure Connection  limeahidi kutoa basi litakalopeleka washiriki na kuwasubiri kwa gharama za Sh 180,000 kwenda na kurudi. Vilevile Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), wanajipanga kuwa na usafiri wa ndege na yapo mashirika mengine ya ndege yanatoa huduma hiyo kwa wafanyabiashara wakubwa wanaotaka kusafiri kwa njia ya anga,” amehakikisha Bw Rutageruka.

Mwenyekiti wa TASWE Saccos, Bibi Anna Matinde, amewahimiza wajasiriamali wa Tanzania kuhudhuria kongamano hilo.

Pichani juu:

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Bw Edwin Rutageruka, akiongea na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo.

Share

clement

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *