Matinde awataka wajasiriamali wachangamkie biashara Burundi

Matinde awataka wajasiriamali wachangamkie biashara Burundi

Na David  Nawepa

Mkurugenzi wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania(TPSF) Bibi Anna Matinde, amewataka wajasiriamali wa Tanzania kuhudhuria kongamano na maonyesho ya biashara yatakayofanyika Burundi kwa sababu maandalizi ya usafiri wa ardhini na anga tayari yamefanywa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo (Septemba 7, 2017) katika ofisi za Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) jijini Dar es Salaam, Bibi Matinde amewahakikishia wajasiriamali kuwa mipango mizuri imefanywa na kwamba wao na mali zao watuwa salama wakati wote wakiwa Burundi.

“Nawaomba wajasiriamali kuchangamkia kongamano na maonyesho haya.  Wenzetu Burundi wanafanya biashara ya vyakula na mavazi na Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo upande wa Mashariki, ukichunguza bidhaa hizo wanazitoa Tanzania lakini kwa njia zisizo rasmi.

“Burundi ina watu milioni 10 na Mashariki ya Kongo kuna watu milioni 10, hilo ni soko la watu milioni 20. Tunalalamika hakuna soko, wakati ndio huu,” amesema Bibi Matinde.

Bibi Matinde, ambaye peia ni Mwenyekiti wa TASWE Saccos, amesema mwenyewe amefanya vikao vingi na wajasiriamali nchini Burundi na kubaini fursa nyingi za kibiashara na amejiridhisha kwamba hali ya usalama inaridhisha.

Ametaja  bidhaa nyingi zinazotakiwa Burundi kuwa  ni nafaka, hasa mahindi, maharage, mchele, unga wa ngano na dagaa. Bidhaa nyingine ni gesi asilia, bidhaa za petroli na vifaa vya ujenzi.

Katika mkutano huo Kaimu Mkurgenzi wa TanTrade, Bwana  Edwin Rutegaruka amewahakikishia wafanyabiashara wanaotaka kuhudhuria kongamano na maonyesho hayo kuwa wasiwe na shaka kuhusu masuala ya forodha wala kodi na vibali vya kufanya biashara nchini Burundi kwa sababu mambo yote hayo yamefanyiwa kazi.

“Tayari tumezungumza na Wizara ya Biashara nchini Burundi vibali vya kufanya biashara vimeshaandaliwa, hivyo bebeni bidhaa zenu. Katika mpango huu tumeshirikiana na TFDA, TBS, Uhamiaji, VAT na TIC kwa hiyo kila kitu kitafanyiwa kazi kulingana na mahitaji,” amesema Bw. Rutegaruka.

Kuhusu suala la usalama Kaimu Mkurugenzi  Mkuu huyo  naye ameeleza kuwa ili kujiridhisha juu ya suala hilo, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imefanya utafiti na kubaini kuwa hali nchini Burundi ni salama.

Kadhalika  Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Bw Rajab Gamaha, naye ameihakikishia TanTrade kuwa Burundi ni salama.

“Balozi Rajab Gamaha anayetuwakilisha Burundi alikuja tukafanya naye mazungumzo: TanTrade na TPA, akatueleza namna fursa za kibiashara na uwekezaji zilivyo nyingi,” ameongeza Bw. Rutegaruka.

Kadhalika Bw. Rutageruka ameeleza kuwa  maandalizi  ya kongamano la kibiashara kati ya Tanzania na Burundi litakalofanyika jijini Bujumbura yako ngazi ya mwisho.

Kongamano hilo litafuatiwa na maonyesho ya biashara yatakayofanyika katika viwanja vya Tempete, amethibitisha.

“Usafiri wa mabasi upo.  Basi la kampuni ya Adventure Connection  limeahidi kutoa basi litakalopeleka washiriki na kuwasubiri kwa gharama za Sh 180,000 kwenda na kurudi. Vilevile Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), wanajipanga kuwa na usafiri wa ndege na yapo mashirika mengine ya ndege yanatoa huduma hiyo kwa wafanyabiashara wakubwa wanaotaka kusafiri kwa njia ya anga,” amehakikisha Bw Rutageruka.

Pichani juu:

Mkurugenzi wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania(TPSF) Bibi Anna Matinde, akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Tan-Trade Jijini Dar es Salaam leo. Mkutano huo uliitishwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Bw Edwin Rutageruka.

 

Share

clement

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *