Kamati ya Bunge Kilimo, Mifugo yaishauri serikali kutoa ruzuku kwa SAGCOT

 

Na Mwandishi Wetu, Njombe
BAADA ya kuridhishwa na utendaji wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Kusini
mwa Tanzania (SAGCOT) katika kongani ya Ihemi katika mikoa ya Iringa
na Njombe, Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na Maji imeshauri
serikali kutoa ruzuku kwa kituo hicho ili kuongeza tija kwa wakulima.

“Iwapo Serikali itatoa ruzuku kwa  SAGCOT  itakiwezesha kituo hicho
kufanya  vizuri zaidi katika kongani hii na nyingine zilizobaki,
nashauri serikali isijitoe katika hili bali iwe karibu  ili wafanye
kazi zao vizuri na kuajiri watu wengi kuongeza utaalamu,” alisema
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati Bw.Mashimba Ndaki wakati wa majumuisho ya
ziara hiyo ya siku tano katika mikoa ya Iringa na Njombe hivi
karibuni.

Bw. Ndaki alibainisha kuwa wameona mambo mengi katika kongani hiyo,
wameona pia namna wazalishaji wanavyosumbuliwa na taasisi nyingi za
serikali wakati wa kukusanya tozo za huduma na bidhaa.

“Naishauri serikali iweke kituo kimoja cha kukusanya tozo na ushuru wa
wawekezaji, tumeona namna inavyowawia vigumu kuwafikia wote, SAGCOT
tayari imefanya kazi yao vizuri kwa kuunganisha sekta ya umma na sekta
binafsi kilichobaki tuwaunge mkono,” alisisitiza na kuonyeshwa
kuridhishwa kwake na kazi za taasisi hiyo.

Alisema Kamati yaken imebaini tatizo jingine la miundombinu hasa ya
barabara wakati  walipokuwa Njombe na namna wakulima wa chai
wanavyolalamika ubovu wa barabara, kwa sababu wanavuna wakati wa mvua
na majani yanatakiwa kufika mapema kiwandai kabla hayajaharibika.

“Kwa kweli ni lazima iliangalie hili wakati huu ambapo tunaazimia kuwa
na uchumi wa kati na viwanda. Zao la chai linastawi vizuri sana katika
kongani hii,” Bw. Ndaki alisisitiza.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Bwana Christopher Ole Sendeka
aliwashukuru wajumbe wa kamati hiyo kwa kutembelea mkoa wake lakini
pia akawaomba warejee tena ili kutembelea wilaya zote na kujionea
fursa za kilimo zilizojaa mkoani humo.

“Naishukuru kamati hii ina uelewa mkubwa katika masuala ya kilimo na
watalamu wangu watayachukua mambo mliyowashauri kwa ajili ya
utekelezaji,” alisema Bw. Ole Sendeka.

Alichukua nafasi hiyo kuishukuru kamati na kuiomba kutembelea mkoa
wake tena ili kuona fursa nyingi za kilimo zilizojaa kila wilaya.
Wananchi wa Njombe katika uzalishaji si wavivu na wanajua kama kuna
tija wanayotafuta.

Awali,  Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT, Bwana Geoffrey  Kirenga baada
ya kuzungumza na wabunge hao kwa muda mrefu kuhusiana na fursa za
kilimo zilizopo kwenye ukanda au ushoroba huo wa nyanda za juu kusini
hatimaye wamepata fursa ya kujionea kwa macho miradi inayoendeshwa kwa
ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma.
“Katika ziara hii kila tulipoanza tulitembelea ofisi za mkuu wa mkoa
husika kwa sababu kazi kubwa zinazofanyika katika maeneo hayo uongozi
wa mkoa na wilaya husaidia kujenga mazingira mazuri ya kibiashara na
hapo ndipo utendaji wa ubia unapoonekana,” alisema Kirenga na
kuongeza:

“Tulipotembelea maeneo ya uwekezaji katika viwanda vya nyama, maziwa
na chakula cha mifugo wajumbe walipata wasaa wa kusikiliza changamoto
wanazokumbana nazo, vilevile wakulima wadogo walipata wasaa wa kutoa
manung’uniko yao. Waliona namna fursa zilizopo lakini pia upande wa
maziwa waliona namna tunavyosindika kwa kiwango kidogo.”

Akizungumzia upande wa uzalishaji viazi katika ukanda huo, Kirenga
alisema uzalishaji mbegu na pembejeo ni suala muhimu katika kilimo
hicho na kubainisha kuwa kwa sasa Tanzania ipo katika ramani ya
uzalishaji viazi duniani.

SAGCOT ni kituo kinachounganisha taasisi za sekta binafsi na sekta ya
umma katika ukanda wa nyanda za juu kusini ambapo imeligawa eneo hilo
katika kongani sita ikiwemo Ihemi, ambapo inaangazia ongezeko la
thamani katika mazao ya nyanya, viazi mviringo, soya na maziwa.

Mwisho

Share

clement

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *