Mratibu mradi wa maji Bagamoyo ngoma nzito

 

David Nawepa, Bagamoyo

Mratibu na msimamizi  wa mradi wa maji unaolenga kuwapa maji safi na salama zaidi ya wananchi 10,000  wa Halmashauri ya  Bagamoyo, Mhandisi Jason Niraphael,  jana (Jumatatu, 30 Oktoba, 2017) amejikwaa  kwa  Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Bw. Kangi Lugola baada ya kutoa maelezo duni  juu ya mradi anaosimamia.

Waziri Mdogo Lugola, ambaye kateuliwa wiki mbili zilizopita, amekataa maelezo haya na kuamuru mhandisi huyo aondolewe kutoka katika mradi huo na kuwekwa muhala kwingine. Kadhalika ametaka apewe taarifa juu ya mradi huo kabla ya juma hili kwisha.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo,   Bw. Majid Mwanga, amesema matatizo ya  mradi huo yamekuwa yakiwaumiza vichwa na wangependa jambo hili lipatiwe ufumbuzi.

Mradi huo unalenga katika kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabianchi kutokana na ongezeko la kina cha bahari.

“Mimi nimekuja hapa kufanya kazi halafu wewe unanijia mikono mitupu,” Waziri Lugola amemweleza  Bw Niraphael ambayeaonekana kutaharuki.

Mhandisi ameeleza kuwa kutokana na sababu zisizowea kuzuilika visima 17 vilivyopangwa kujengwa sasa vitapungua na kuwa 10 na matanki ya kuhifadhia maji ya mvua yatapungua kutoka matano hadi mawili na matanki hayo yatawekwa shule za sekondari za Kingani na Matipwili.

Bw Lugola, ambaye tayari ametembelea  maeneo mengi kuangali athari za mabadiliko ya tabianchi na uchafuzi wa mazingira kwa sababu ya kutupwa taka ngumu katika vyanzo vya maji, amekataa taarifa ya mhandisi huyo na kusema huo ni kati ya miradi mibovu aliyopata kushuhudia katika maisha yake.

“Haya mambo ndiyo yanayoturudisha nyuma. Nilitoa taarifa mapema kuwa ninakuja, nilitegemea kukuta umejipanga. Hii miradi inagharimu pesa nyingi lazima itekelezwe kwa wakati ili wananchi wanufaike,” amesema Bw Lugola na kuonya kwamba serekali haitawaonea huruma watendaji wanaozembea katika utekelezaji miradi muhimu.

Naibu waziri ameshauri miradi ya mazingira isimamiwe halmashauri za wilaya huko inakotekelezwa kwa kuwa halmashauri ndizo zinazojua matatizo ya wananchi, vipaumbele vyao na zina wataalamu wa kutekeleza miradi hiyo.

Bw Lugola ameonyesha kukerwa na  mkanganyiko  kwenye taarifa ya mafunzo yanayodaiwa kutolewa na taasisi mbalimbali wilayani humo. Fungu kwa ajili ya mafunzo kwa taasisi ili kuelewa umuhimu wa kuhifadhi mazingira lilitengewa zaidi ya shilingi milioni 85.

Mradi huo unatarajiwa kugharimu shilingi milioni 912 na unasimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.   Mradi huo ulifanyiwa  tathmini tangu mwaka 2012, utekelezaji ulianza Januari 2015.

Wakati huo lengo lilikuwa ni kuchimba visima 17 na kujenga matanki ya kuhifadhi maji ya mvua katika taasisi tano za serikali.

Lakini paka  sasa kazi iliyofanyika ni kidogo wakati mradi umepangwa ukamilike Februari, mwakani, miezi 4 kutoka sasa.

Mkurugenzi wa Halmshauri ya Bagamoyo, Bi. Fatuma Latu, baada ya kupokea agizo la naibu waziri  ameeleza kwamba halmashauri haipewi taarifa sahihi na kumhakikishia kwamba halmashauri si wasimamizi wa mradi huo.  “Sisi si wasimamizi bali tunaonyesha njia tu ndio mana hatujui chochote.”

Bi Latu ameongeza: “Tumesimamia miradi mingi yenye gharama kubwa zaidi ya huu na imekamilika vizuri, nadhani ipo haja ya kushirikishwa kwa undani ili tujue namna ya kuukamilisha kwa mafanikio kwa sababu huu ni mradi wenye nia njema kwa wakazi wa Bagamoyo.”

Bw.  Mwanga, ameahidi kuwa ofisi yake itafuatilia vikundi vyote vilivyotajwa kuwa vimepewa mafunzo ili kujua kama vina uelewa wowote kuhusiana na mambo ya mazingira au wameingizwa tu kiujanja.

“Mheshimiwa nakuhakikishia hili jukumu ulilonikabidhi ni dogo kwangu lipo ndani ya uwezo wangu, ndani ya siku chache nitakuletea taarifa iliyokamilika. Hata sisi hili suala linatuumiza kichwa tunataka likamilike, nakuahidi kila kitu kitakuwa sawa,” amesema Bw Mwanga.

Mwisho//bb

Share

clement

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *